5 Juni 2025 - 15:56
Source: Parstoday
Trump na matakwa ya kupindukia kwa Iran: Je, Washington inataka kufikia makubaliano au kutwisha matakwa?

Rais Donald Trump wa Marekani amekariri matakwa ya kupindukia mipaka ya Washington kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran kwa ajili ya kufikiwa mapatano ya pande mbili.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijami hapo siku ya Jumatatu, Juni 2, Trump alikariri madai yake na ya maafisa wengine wa Marekani kwa kuandika: "Hatutaruhusu urutubishaji wowote wa urani kwenye makubaliano yanayoweza kufikiwa kati ya pande mbili!"

Kauli za hivi karibuni za Trump zinaweza kutathminiwa kuwa ni marudio ya madai ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na maafisa wa utawala wake, akiwemo Steve Whitkoff, mjumbe wake maalum katika masuala ya Asia Magharibi.

Licha ya kufanyika duru tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, utawala wa Trump unaendelea kukariri kauli, madai na vitendo vyake vinavyogongana huku ukitoa wito wa kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja. Kwa upande mmoja, wanajaribu kuwasilisha sura chanya ya mazungumzo yao na Iran, na kwa upande mwingine, kwa kurudia madai na vitisho vya Washington katika fremu ya siasa za mashinikizo ya juu kabisa na uchochezi dhidi ya Iran, wanajaribu kujenga hofu kuhusu matokeo ya kutofikiwa makubaliano.

Kuhusiana na hili, Carolyn Levitt, msemaji wa Ikulu ya Marekani alisema katika mkutano na waandishi wa habari mnamo Jumanne, Juni 3 kwamba Steve Whitkoff alituma pendekezo la kina kwa Iran kuhusu makubaliano ya nyuklia, na kuwa Rais Trump anatumai kuwa pendekezo hilo litakubaliwa. Kwa mara nyingine ametumia lugha ya vitisho, kwa kusema: "Ikiwa pendekezo la Whitkoff halitakubaliwa, Iran itakabiliwa na matokeo makali."!

Tunaweza kusema kuwa jibu la Iran kwa vitisho hivyo vya Marekani limebainishwa wazi na Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran. Araqchi alisema katika uzinduzi wa kitabu chake kinachoitwa "Nguvu ya Majadiliano" nchini Lebanon kuwa: "Kama tusingekuwa na nguvu zinazohitajika za kujilinda na Marekani kuwa na nguvu ya kuvishambulia kwa mabomu vituo vyetu vya nyuklia, kusingekuwa na sababu ya kuingia katika mazungumzo. Ikiwa hatungekuwa na nguvu za kisayansi na hatungeweza kuendelea na mpango wetu wa nyuklia, kusingekuwa na sababu ya kufanya mazungumzo."

Trump na matakwa ya kupindukia kwa Iran: Je, Washington inataka kufikia makubaliano au kutwisha matakwa?

Trump na Steve Whitkoff

Siku ya Jumamosi, Mei 31, Badr Busaidi Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman aliwasilisha kwa Abbas Araqchi  Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pendekezo rasmi kutoka kwa serikali ya Marekani kuhusu mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja wakati wa safari yake ya saa chache mjini Tehran. Safari hiyo, ambayo ilikuwa sehemu ya upatanishi wa Oman kati ya Tehran na Washington, ilikusudiwa kuwasilisha "vipengele" vya pendekezo la Marekani kwa Iran. Kisha Araghchi aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba Iran itajibu ipasavyo pendekezo hilo "ndani ya mfumo wa kanuni zake, maslahi ya taifa na haki za watu wa Iran."

Katika safari yake ya hivi karibuni nchini Misri, Araqchi alisema kuwa pendekezo hilo la Marekani, lilikuwa na utata na maswali mengi ambapo masuala mengi yaliyogusiwa kwenye pendekezo hilo hayakufafanuliwa wazi.

Ni wazi kuwa suala muhimu na la msingi katika mzozo wa Iran na Marekani ni suala la kuendelea kurutubishwa urani katika ardhi ya Iran. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inachukulia urutubishaji kuwa haki yake isiyoweza kupokonywa ndani ya fremu ya sheria za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), hivyo haikubali kabisa siasa zisizo za mantiki za Marekani za kuilazimisha isimamishe urutubishaji huo. Hii ni katika hali ambayo Trump na utawala wake kupitia sera ya "amani kupitia nguvu," wanadhani kwamba wataweza kuishinikiza Iran ikubali siasa hizo kwa kuiwekea vikwazo vikali kwa upande mmoja na kutishia kuishambulia kijeshi kwa upande wa pili. Wakati huohuo, wakati wa muhula wake wa kwanza kama rais, Trump mwenyewe alitumia siasa hizo hizo za mashinikizo ya juu dhidi ya Iran, na kuiwekea vikwazo vya kila aina, lakini akashindwa kufikia lengo lake la kusimamisha mpango wa amani wa nyuklia wa Iran. Hivyo, ikiwa kweli Trump anataka kufikia makubaliano na Iran, ni lazima sio tu arekebishe mtazamo wake kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran bali pia asahihishe matakwa yake na kuyafanya yaendane na misingi ya busara.

Kwa upande mwingine, msimamo wa Tehran kuhusu suala la kurutubisha urani umebainishwa wazi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, ambapo amesema kwamba "Kuendelea kurutubisha urani katika ardhi ya Iran ni mstari mwekundu kwa taifa la Iran, na huu ni ukweli usiopingika ambao inaonekana kwamba nchi zote sasa zimeukubali." Wananchi wa Iran wamejitolea muhanga pakubwa katika kufikia fahari hii ya kitaifa na wamevumilia vikwazo vizito vya Marekani kwa zaidi ya miaka 20 ili kufikia mafanikio haya ya wanasayansi wao. Ameongeza kwa kusema: "Hata hivyo, tuko tayari kuchukua hatua katika kujenga imani ili kuhakikisha kwamba urutubishaji huu haupelekei kutengenezwa silaha za nyuklia.

Mpira sasa uko kwenye uwanja wa Marekani, na ikiwa Washington inataka kweli kufikia makubaliano ya nyuklia na Tehran, lazima iwe na mtazamo sahihi kuhusu hali halisi ya mambo inapocheza na Iran mchezo wa kuziwezesha pande zote mbili zifikie malengo yao.

Your Comment

You are replying to: .
captcha